Loading...

Chuo cha Sanad kimempokea Mlinganiaji kutoka Indonesia, Shekhe Buya Yahya, na Kujadili Fursa za Ushirikiano wa Kielimu na Kuanzishwa masomo ya Sanad kwa lugha ya Kiindonesia

16/11/2026
Matembezi

Katika juhudi za kupanua wigo wa shughuli zake za kielimu na ushirikiano wake katika eneo la Kusini Mashariki mwa Asia, Chuo cha Sanad cha Elimu za Sharia kilimpokea Mlinganiaje kutoka Indonesia, Shekhe Yahya Zainul Maarif Majzuriy, anayejulikana nchini Indonesia kwa jina la Shekhe Buya Yahya. Na hilo ni katika ziara iliyolenga kukifahamu Chuo cha Sanad na programu zake za kielimu, pamoja na kujadili fursa za ushirikiano wa kielimu na kitaasisi kati ya pande hizo mbili.
Mazungumzo hayo yalihusu utambulisho wa ujumbe na dira ya kielimu ya Chuo cha Sanad, pamoja na programu zake zinazoendana na mtaala wa Darul Mustafa ya Tarim, katika masomo ya Kiislamu, na mfumo wake wa elimu ya kidijitali unaolenga kufikisha elimu za Sharia katika jamii na nchi mbalimbali, pamoja na kuchunguza fursa za kushirikiana katika kuendeleza programu za kielimu na kupanua wigo wa manufaa yake nchini Indonesia.
Pande hizo mbili pia zilijadili kuhusu kuandaa masomo ya Chuo cha Sanad kwa lugha ya Kiindonesia na kuyawezesha kwa wazungumzaji wa lugha hiyo. Hili ni hatua muhimu katika kupanua wigo wa elimu ya Sharia kwa njia ya kidijitali na kunufaika nayo kiulinganiaji kupitia Taasisi zilizopo nchini Indonesia. Jambo hili litachangia kufikisha elimu halisi ya Sharia kwa watu wengi zaidi wanaopenda elimu.
Umuhimu wa ushirikiano huu unatokana na nafasi aliyonayo Shekhe Buya Yahya kielimu na ulinganiaji nchini Indonesia, pamoja na uzoefu wake mkubwa katika nyanja za elimu, malezi na kulingania. Shekhe huyo alianzisha taasisi ya Al-Bahjah, inayojumuisha idadi ya Vyuo vya Kiislamu, Shule na Chuo Kikuu, sambamba na Vituo kadhaa vya Redio katika Miji mbalimbali ya Indonesia na Kituo cha Televisheni cha Al-Bahjah (Al-Bahjah TV). Vilevile, ana mchango mkubwa wa kielimu kupitia vitabu alivyoandika kwa lugha ya Kiarabu na Kiindonesia.
Ikumbukwe kuwa Shekhe Buya Yahya atakuwa miongoni mwa walimu watakaoshiriki kufundisha kwa lugha ya Kiindonesia katika Chuo cha Sanad. Jambo hili litaimarisha uwepo wake wa kielimu na kuunga mkono juhudi zake za kutoa maudhui ya kielimu ya Sharia yanayounganisha uhalisia wa misingi ya elimu na kuzingatia mahitaji ya jamii ya Kiindonesia.
Chuo cha Sanad kinatarajia ziara hii itakuwa hatua ya vitendo kuelekea kujenga ushirikiano wenye manufaa endelevu, utakaofungua milango mipya ya kuhudumia na kueneza elimu ya Sharia, pamoja na kuimarisha nafasi ya taasisi za kielimu katika ulimwengu wa elimu ya kidijitali. Hayo yakianzia Tarim na kuenea sehemu kubwa ya ulimwengu wa Kiislamu.
Shekhe Buya Yahya alipokelewa na Ustadh Ahmad Saad Khatib, Mkurugenzi Mtendaji wa Chuo cha Sanad. Aidha, Sayyid Hamid bin Umar bin Hafidh, Msimamizi wa Masuala ya Kielimu katika Chuo hicho, alishiriki katika mazungumzo hayo kwa njia ya mtandao. Katika kikao hicho, walibadilishana mawazo kuhusu maeneo yanayowezekana kushirikiana na namna ya kunufaika na uzoefu wa kielimu na kitaasisi kwa pande zote mbili.